CHENGE: HATUCHAGUI VIONGOZI WA KUBEBA ZEGE
https://alloycenyanda.blogspot.com/2015/10/chenge-hatuchagui-viongozi-wa-kubeba.html
Mbunge wa Bariadi Andrew Chenge (CCM) amewataka wananchi wa
jimbo lake kuchagua viongozi wenye sifa za uongozi na si vinginevyo.
Mh. Chenge alitoa kauli hiyo alipowahutubia wananchi wa kata
ya Bunamhala jimbo la Bariadi leo Jumanne katika mkutano aliouita wa lala
salama kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu siku ya jumapili.
“Nataka mchague viongozi wenye upeo wa mambo, wazoefu na
wenye hoja za ushawishi kama mimi, msichague viongozi kwa kuangalia nguvu na
vifua vikubwa uongozi sio mashindano ya mbio za baiskeli wala kubeba
zege”Alisema Chenge kauli iliyoacha minong’ono miongoni mwa wananchi.
Mbali na kauli hiyo Mbunge huyo anayewania muhula wa tatu
kuliongoza jimbo la Bariadi aliwaomba wanachi waliohudhuria mkutano huo
kuhakikisha wanampa kura za kutosha ili akamilishe mambo aliyabakiza katika
ahadi zake huku akitoa ahadi nyingine za kuboresha huduma za afya, miundombinu
na elimu.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walimwomba
mbunge huyo kuhakikisha anawasaidia kuondokana na umaskini na kuwaletea
maendeleo zaidi jambo ambalo Mh. Chenge alisema atalishughulikia kama
watamchagua tena huku akiwataka wananchi kuwa na subira kwa baadhi ya mambo
kwani mambo mazuri hayataki haraka.
(Mbunge wa Bariadi Andrew Chenge akiwa katika mkutano wa
hadhara kata ya Bunamhala jimboni hapo)
Na, Aloyce Mchunga
Na, Aloyce Mchunga
