Tanzania inaongoza kwa Wagonjwa wa Saratani ya Mlango wa kizazi Afrika Mashariki.
https://alloycenyanda.blogspot.com/2015/10/tanzania-inaongoza-kwa-wagonjwa-wa.html
MANSOUR JUMANNE, MWANZA.
TAASISI ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) imesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa
ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi Afrika Mashariki.
Imeelezwa
kuwa hali hiyo inaonatokana kusababishwa na hali ya umaskini walionao Watanzania
wengi, uelewa mdogo pamoja na mila potofu juu ya ugonjwa huo.
Akisoma
taarifa ya WAMA, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza Dk. James Kengia alisema hayo jana jijini hapa wakati akifungua mafunzo
ya kuhamasisha timu za afya za Wilaya za Mikoa ya Mwanza, kuhusu namna ya kupambana na saratani ya
mlango wa kizazi.
“Takwimu za
ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kwa Tanzania zinasikitisha sana. Tunaarifiwa
kwamba idadi ya wanawake 6,241 hugundulika kuwa na saratani kwa mwaka.
“Kati yao wanawake
4,355 hufariki kila mwaka katika nchi za Afrika Mashariki….Tanzania inaongoza
kwa wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi,” alisema DK. Kengia.
Naye Mkurugezi wa Uboreshaji wa Afya wa Taasisis hiyo
WAMA, Dk. Sarah Maongezi alisema wagonjwa wengi wa ugonjwa huo, wanafika
hospitali wamechelewa hali inayosababisha wagonjwa wengi kufariki dunia.
Kufuatia
hali hiyo, aliwataka wanawake kupima mapema afya zao ili kujua iwapo wana
tatizo lolote la kiafya na baadaye wawahi matibabu.
“Karibia
wanawake 6,000 hufika katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road, lakini kati ya
hao wanawake 4,000, hufariki dunia baada ya miezi mitatu kutokana na kuchelewa
matibabu.
“Hivyo wanawake
wasisubiri hadi dalili bali pindi waonapo vituo vinavyopima basi wafike
wakapime afya zao,” alisema Dk. Maongezi.
Akizungumza
kwa niaba ya watoa huduma wa saratani ya mlango wa kizazi waliohudhulia mafunzo
hayo, Dk. Jaliath Lange kutoka Chama Cha Madaktari Wanawake (MEWATA) alisema
wametoa mafunzo kwa madaktari wa Mkoa wa Mwanza jinsi ya kupima na kutibu
ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.
“Kwa upande
wa Mkoa Mwanza tunataka tuurudishe huu mpango katika ngazi ya jamii, katika
vijiji na wilayani ili tujue kama tatizo limeongezeka au linapungua,” alisema
Dk. Lange.

