HALI YA KISIASA MKOANI KIGOMA.





MWANDISHI: JUMA SHABANI
MAHALI: KIGOMA.

Hii ni makala maalumu ya kiasiasa kuelekea uchaguzi mkuu ambao utachambua kwa kina hali ya kisiasa mkoani hapa kwa kila Nyanja huku tukipitia matukio ya nyuma kama kioo cha kuangalia nini kitatokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Makala hii itaangazia kwa ujumla hali ilivyo sasa kisiasa na ilivyokuwa na kuakisi matarajio ya wananchi wa Kigoma katika uchaguzi huu. Makala hii itachunguza kwa kina ubora wa sera, wagombea na uelewa wa wananchi katika kufikia jukumu kubwa la kuchagua hapo Oktoba 25, 2015.

MKOA WA KIGOMA KWA UJUMLA.
Mkoa wa Kigoma una ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 45,066 sawa na asilimia 4.8 ya eneo lpte katika jamuhuri ya muungano wa Tanzania. Kulingana na sense ya mwaka 2012, mkoa wa Kigoma una wananchi wanaofikia 2,127,930.

Mkoa wa Kigoma una wilaya za Kigoma, Uvinza, Kasulu, Buhigwe, Kibondo na Kakonko. Mkoa huu una majimbo ya Kigoma Mjini, Buhigwe {Manyovu}, Kasulu Vijijini, Kasulu Mjini, Buyungu, Muhambwe, Kigoma Kaskazini na Kigoma Kusini. Mkoa wa Kigoma una kata 139 zenye wapiga kura 774,941.

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, Mkoa wa Kigoma uliandikisha wapiga kura 774,941 sawa na 83% ya makadirio ya tume ambayo ni sawa na 75.1% ya makisio ya NBS.

MKOA WA KIGOMA NA HISTORIA YA UCHAGUZI WA VYAMA VINGI.
Mkoa wa Kigoma ni mkoa wa mwanzo kabisa kufanya siasa za vyama vingi mapema mwaka 1994 baada ya uchaguzi mdogo ulifanywa mwaka huo baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini  Ibrahim Mbano kufariki dunia.
Huu ndio uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kufanyika ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa jaribio la aina mpya siasa mjini. Katika uchaguzi huu mambo kadhaa yalijitokeza ambapo Dr. Aman walid Kabourou aliingia kwa mara ya kwanza kwenye siasa akitokea nchini marekeni. Uchaguzi huo pamoja na kushirikisha vyama vingi ila ni vyama vya CCM na Chadema vilivyokuwa na ushindani wa hali ya juu ambapo kwa CCM alisimamishwa Ndugu Azim dewji na kwa Chadema alisimamishwa Kabourou.
Matokeo ya uchaguzi huo yalionesha ishara njema kwa siasa za vyama vingi ambapo CCM ilishinda kwa kura chache sana na Chadema kupitia Kabourou walikwenda mahakamani kupinga ambapo uchaguzi ulitenguliwa kabla ya Azim kukata rufaa. Kwakuwa mwaka 1995 ulikuwa unakaribia na uchaguzi mkuu kuitishwa, hivyo jimbo lilikaa bila mbunge kwa mwaka wa 1994 maana kesi ilikuwa mahakama ya rufaa.

Mwaka 1995 ilikuwa mwaka wa kwanza wa uchaguzi mkuu wa vyama vingi ambapo kwa Kigoma tayari kulikuwa na uzoefu wa siasa za vyama vingi. Wakatai wengine wanaanza kuona faida na hasara ya siasa za vyama vingi, kwa Kigoma hakukuwa na jipya sana. Watu kwa makundi walikuwa na kesi za uchagu, wengine walishapigwa na polisi na mambo kadhaa ya kisiasa za ushindani yakiwa yameshaonekana.

Pamoja na kuwa kulikuwa na vyama vingi sana vilivyosimamisha wagombea mkoani hapa zaidi ya mikoa mingi nchi hali iliyoashiria kupokelewa kwa vyama vingi mkoani ila vyama viwili vya CCM na Chadema ndio vilikuwa na nguvu mkoani hapa. Ni kipindi hiki ambapo wanakigoma walipokea mabadiliko chini ya NCCR na Mrema katika ngazi ya Urais ila walibaki na misimamo katika vyama vyao vya CCM na Chadema. Kwa ngazi ya ubunge, mara ya kwanza Mkoani hapa jimbo la Kigoma Mjini lilipata mbunge wa upinzani huku kata nyingi pia zikienda upinzani.

Hali ya kisiasa mkoani Kigoma imekuwa haitabiliki ambapo katika majimbo mengi upinzani na CCM wamekuwa wakipokezana kuongoza. Mfano wa majimbo hayo ni Kigoma Mjini, Kigoma Kusini, Kigoma Kaskazini na mwaka 2010 majimbo ya Kaulu na Kibondo Mjini yalichagua upinzani kwa mara ya kwanza.

CCM imebaki kuwa chama chenye nguvu mkoani humu ambapo kura za urais kwa miaka yote zimekuwa zikiongozwa na CCM, huku wabunge wengi wa jimbo hili wakitokea CCM. Pia, mkoa huu umebahatika kutoa mawaziri na manaibu mawaziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MUAMKO WA WANANCHI
Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na muamko wa hali ya juu ambapo mkoani hapa kumekuwepo na vyama vinne vyenye nguvu ya kiushindani. Vyama hivyo ni CCM, Chadema, ACT na NCCR Mageuzi. Hivyo kwa mara ya kwanza kama alivyosema Mh, Mbowe mwenyekiti wa Chadema na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa alipoiona hali ya kisiasa mkoani Kigoma alisema “Natambua mwaka huu hapa kuna ngoma nzito”

Makala hii inasitishwa hapa kwa leo. Mwisho wa makala hii kwa leo ni mwanzo wa makala nyingine kesho ambapo nitaanza kuchambua kwa kina hali ya kisiasa ilivyo kuelekea uchaguzi mkuu 2015 katika ngazi ya Urais.




Related

Tanzania 4192134151518081706

Post a Comment

emo-but-icon

Tafuta Habari

Wasomaji

Tufuatilie Facebook

Maoni Yako

Name

Email *

Message *

item
Wordpress